Mohammmed Ali: Jicho Pevu- Barua kwa Naibu Rais William Ruto

Mohammmed Ali: Jicho Pevu- Barua kwa Naibu Rais William Ruto
Mohammmed Ali: Jicho Pevu- Barua kwa Naibu Rais William Ruto

Hujambo Bwana Kusema na Kutenda, naomba safari hii, kabla hujatenda, nikujulishe mawili hivi. Najua huna raha, hupati usingizi na unahofia maisha yako licha ya utajiri uliyonayo.

Leo hii umejipata kubanwa na uliowaamini. Ndoa za haraka na tamaa zina shida Bwana Ruto. Ukipenda viazi, usiogope mimba, ndio msemo wetu kule vilima vya raha. Ndoa yako na Uhuru Kenyatta imefikia kiwango cha mtu mmoja kati yenu kupata mimba. Si mimba ya mtoto, bali mimba ya machungu na kusalitiana.

Miaka ya nyuma, kabla ya wewe kuwa β€˜hustler’ wa kizazi kipya, niliwahi kukutembelea mara kwa mara katika afisi zako katika jumba la Transcom.

Tulizungumza na kutaniana na hata kuzungumza kwa simu. Ulikuwa machachari na mtu wa watu. Mwaka wa 2007/2008 baada ya ghasia za baada ya uchaguzi, wewe na Raila mlikuwa chanda na pete mkijaribu kuunda serikali ya muungano na kupigania nafasi ya ukubwa wa wana odm katika serikali hiyo iliyowaibia kura.

Katika pilka pilka hizo, usaliti wa hali ya juu ulitendeka. Wabakaji wa demokrasia walianza kunoa kisu huku nyinyi mkidhani mambo yalikuwa yashakwisha.

Wacha niseme TNA kwa sababu URP haina usemi tena. URP imebakwa peupe wazi wazi. URP inalea mimba haramu, mimba ya kujitakia. William Ruto usidanganywe na maombi za kinafiki zinazotekelezwa na wafuasi na maadui wako. Kama unataka kutatua shida zako binafsi na maombi tasa, pole.

Maombi ni ya kuondoa usinzi, wanaofumaniwa na wake za watu, mapepo na kumshukuru Mungu na kumwogopa, sio safari za mahakamani.

Kenya imekuwa taifa la kuzalisha wanafiki na watu waoga. Tumekubali ukiritimba itawale. Profesa hana tofauti na mtoto wa darasa la kwanza. Jiepushe na wanaokuzunguka na kujifanya wasomi ila ni watu wa maslahi. Maji tayari yamemwagika lakini ni wewe kuamua mkondo wa maji hayo.

Huna budi kurudi kwa marafiki zako wa zamani, kwani tayari Wakenya washajua kikulacho ki nguoni mwako. Kwa maoni yangu binafsi, na naomba unikosoe, ni wewe kujiondoa mara moja kwenye muungano wa kinafiki. Warudie uliowakosea na uombe msamaha. Hakika Mungu anatuamrisha kuwasamehe maadui.

Najua ni aibu kwako, lakini kumbuka una familia. Aidha usiwahi kuwaona ama uishi bila ya kuwaona. Uamuzi umo mikononi mwako. Kuna uwezekano wa kujifunza na haya na kuamua kuunda muungano wa ukombozi wa tatu kina nyinyi mkiwa nyuma muwaachie vijana usukani.

Kuna ile kadi moja ya mwisho ya wewe kuwatumia wana URP kupasisha mswaada na wana Cord wa kumwondoa Uhuru Kenyatta mamlakani kwa wingi wa kura bungeni. Lakini kwa yale umewafanyia Wakenya miaka mitatu, sioni kama Cord itakubali uwe Rais kwa miaka miwili iliyosalia kwa mujibu wa katiba ya Kenya.

Bwana Ruto, huu ni wakati wako wakuwaza na kuwazua. Tunazo changamatoto zinazotukabili kama taifa. Badala ya kukaa na kujiuliza kwa nini tuko hapa na tutatoka vipi, tunakaa na kuongea mambo ya kinafiki na ukabila.

Akili ndogo kutawala akili kubwa. Watu wenye akili kubwa wanaweka akili zao mfukoni kwa sababu ya ushabiki wa kivyama badala ya kukaa na kutatua matatizo ya Wakenya. Bunge limekuwa bunge la kitoto. Wakenya sasa wanataka bunge la mapinduzi. Badala ya kuwazomea wakenya waskilizeni.

Advertisements

Leave a Reply

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s